Thursday, February 23, 2006

Taswira ya Utamaduni wa Mwafrika.

Ilikuwa siku ya Jumatano tarehe 23, Februari hapa Illinois ndani ya Chuo cha Magavana ninapofundisha lugha ya kiswahili na utamaduni wa mtanzania nilipobahatika kujuwa nini utamaduni wa mwafrika kwa hawa wenzetu. Wakiwa na mabango makubwa kwenye malango ya chuo hiki niliona maandishi ya kiingereza yasemayo "African Cultural Heritage Day". Kusema kweli sikufahamu nini kinachoendelea juu ya hili.Baada ya kuonana na bosi wangu katika programu hii ya lugha za kimataifa, alinipokea kwa furaha huku akiniambia nisikose siku hiyo kuhudhuria kana kwamba angeweza kuniambia ni heri nikosa mguu mmoja badala ya kuikosa siku hiyo.Hapo ilikuwa siku moja kabla ya tarehe hiyo nilipotonywa na huyo mkubwa wangu.

Kwa bahati nzuri siku hiyo ilikwenda sambamba na siku ambayo mimi na mwenzangu kutoka Nigeria huwa tunakuwa na darasa la kufundisha Riwaya za Kiafrika au kama sikosei kwa king'eng'e inajulikana kama "Afrcan Novels". Kama kawa maprofu tulikusanya madesa yetu kuelekea kunako klasi huku tukitaraji kukuta madenti wakiwa wanatusubiria. Hamadi kuingia tukakuatana na ujumbe unaotuambia kwamba wamekwenda huko kwenye african cultural heritage na wangerudi ndani ya kitambo kifupi. Baada ya mda walirudi tukaendelea na darasa huku mwenzangu akichambua maudhui ya riwaya za kiafrika kwa kuelezea ni jinsi gani zilivyobadilika kulingana na wakati akimaanisha kabla ya ukoloni , wakati wa ukoloni na baada ya ukoloni. Wakati wa mapumziko kama ilivyo ada ya ufundishaji wa huku, mkuu wetu akashauri twende kwenye manesho hayo tuyarishe macho yetu urithi wa utamaduni wa mwafrika.

Asalale!Nilipigwa na bumbuwazi kukuta maonesho hayo yametawaliwa na picha za kizamani. Nyingi yazo zikiwa ni zile zilizopigwa na "manthropolostisi" kabla ya mwaka 1935.Picha hizo zilimwonyesha mwafrika wa kike kwa dharau sana huku matiti yake yakiwa nje na sehemu zake nyeti zikiwa zimefunikwa na kipande cha ngozi. Wanawake wengine walionekana wakiwa na nyuso zilizopakwa rangi na kuchanjwa au kutengeneza michirizi usoni mwao na mwili mzima. Ndugu zangu wasomaji ni kwamba picha hizo zote zinaonekana kuchukuliwa kutoka eneo moja la afrika ya kati hasa Congo Brazzaville (Kongo kwa sasa) na Congo Kinshasa(Zaire au DRC kwa sasa). Kama ilivyo ada ya hawa wenzetu na uwezo wao mdogo wa kufahamu nini kinachoendelea nje ya nchi hii walianza maswali mbali mbali ya kutaka kufahamu nini hasa kinaendelea maeneo haya. Rafiki yangu kutoka Nigeria alikuwa wa kwanza kuulizwa swali akasema kwanza hizi picha si za kweli inaonekana mtu aliwalazimisha kujiandaa kupiga picha ukizingatia kilikuwa kipindi cha ukoloni. Akwaambia ona msichana huyu anavyoangalia, unaona kwamba kabisa anaambiwa na mtu mbele yake kaa hivi. Mimi nikaongezea kwa kusema, picha hizi zimetoka katika sehemu moja ya Afrika japokuwa siamini kama ni za kweli, ila ninachofahamu hamwezi kujumuisha mambo kwa kutumia nchi mbili tu.Hii yote ni kupotosha utamaduni wa bara zima kwa kuleta picha na vitu vinavyowaonyesha wakiwa uchi tu.

Baya zaidi ni hawa wenzangu weusi walionitangulia kuja huku. Eti Afican-Americans?Mimi na wao tunatofautishwa na mda tu. Wao babu zao walikuja wakiwa wamepangwa kwenye majahazi kama nafaka na mimi nimekuja kwa hiari tena ndani ya ndege.Lakini ukiangalia walivyokuwa wanadhihaki na kushangaa hizo picha utafikiri wao hawakutokea huko.

Baada ya matembezi hayo tulirudi darasani kuendelea na kipindi.Kabla ya hapo, tukaongelea ju ya maonesho hayo huku huyo profesa mwenye asili ya kiafrka na anayeonekana kuelewa asili yake akisema kuwa huwezi kusema ndivyo ulivyo utamaduni wa mwafrika kwa ujumla.Akasema huo ni upotoshwaji wa utajiri wa utamaduni wa mwafrika.Hii ilinikumbusha niliposoma kwenye blogu ya Jeff na hasa makala ya jamaa mmoja anaitwa Wainaina niliona mtazamo wa hii mijitu juu ya bara letu. Kwa hiyo nami nilimweleza rafiki yangu kwamba ndiyo maana tulipokwenda kutembelea Museum moja mjini Chicago kwa upande wa Afrika tuliona wanyama tu na sehemu kidogo ya mapishi vikiwa ndo viwakilishi vya tamaduni za bara letu.Nilipojaribu kuowanisha na makala hiyo nikajiuliza,watu hawa wanapeleka wapio utamaduni wetu?Nini hasa chanzo cha uharibifu wa utamaduni huu mzuri na wa aina yake?Na lini hawa watu wataacha kuharibu mama wa ustaarabu wa mwanadamu hasa mbele ya hiki kizazi chao chenye laana?

Asalaam alaykum!.

Sunday, February 05, 2006

Mnyama Msumbufu.

Je, Unamfahamu mnyama msumbufu? Majawabu mbali mbali yaweza kutolewa yupi ni mnyama msumbufu kuliko wote hasa kwa wale wafugwao.Jibu la haraka mtu aweza kusema ni mbuzi kwa wale waliowahi kukaa vijijini wakakumbana na shughuli za kuchunga mnyama huyu wanalifahamu vizuri hilo. Anajulikana kama mbuzi japokuwa ndugu yangu Mwaipopo kwao anajulikana kama mbusi.Kwa wale "maboni tawuni", nasema kumradhi sana kwani mtakuwa hamuelewi purukushani za huyu mnyama isipokuwa mnamfahamu katika mahadhi ya kimapishi hasa kupitia kitoweo chake muruwa.
Kwa upande mwingine binadamu kama kiumbe alipewa uwezo na akili za utashi ni kiumbe msumbufu kuliko vyote.Pamoja na akili yake, kiumbe huyu haridhiki na kila hali aliyonayo.Nikianzia na mimi nilipokuwa Dar es Salaam nilikuwa nalalamika joto na kulala bila hata kujifunika.Hali hii ilisababisha malalamiko makubwa sana kiasi kwamba hata wakati mwingine nilisahau kwamba mambo haya ni ya asili na kuna mtu aliye na nguvu za kufanya marekebisho na hivyo kukufuru mda wote.Hamadi nikapata hii fursa ya kuja huku Steti kama panavyojulikana kule bongo kwa kupatukuza.Wakaniambia nitakuta baridi kali hadi barafu nikasema itakuwa vizuri manake hili juwa lilikuwa linakaribia kunitowa roho.Nilipotuwa huku tabu ikaanza mwanetu mimi nimeonea wapi barafu nchi kavu!Malalamiko yakaanza.Baridi imezidi maisha yangu yako hatarini.Wenyeji wkaniambia hujaona baridi bado!Ipo inakuja na utasimulia hadi vizazi vyako.Nikasema , "Nfwile mwana gwa kyala".Hapo binadamu nikaonekana kumsumbuwa aliyenijalia kuja huku.
Katika hali nyingine ya kushangaza wapendwa wanablogu, nikwamba mnajuwa kuwa bongo imekumbwa na janga la ukame ulioambatana na njaa.Ukame huu umesababisha matatizo makubwa sana kama ukosefu wa chakula cha kutosha na umeme wa mgawo ambao kama ndugu yangu Makene na Lubuva wangekuwepo ingekuwa patashika nguo kuchanika. Hali hii ya ukame iliwapa watu wa kila aina mchecheto hasa ukizingatia njaa ndiyo ilikuwa inatesa jamii kila upande wa nchi.Ni juzi tu watu walikusanyika pale VIWANJAVYA JANGWANI kumuomba Mwenyezi Mungu awajaalie mvua.Cha kushangaza mvua imeanza kunyesha kwa staili ya viroba na sasa binadamu msumbufu kaanza kulalamika kwamba mafuriko yamezikosesha familia makazi huko Tabora.Ewe binadamu kiumbe msumbufu usiyeridhika, kipi bora jua au mvua?

Thursday, February 02, 2006

Mbinu Mpya ya Majambazi Tanzania.

Katika hali ya kustaajabisha, watu wamebaki wamejishika tama huku wakijiuliza kulikoni ndani ya serikali hii iliyoingia na falsafa ya ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. Ikumbukwe kwamba falsafa za namna hii zimekuwa kama kichocheo cha uharifu ndani ya jamii zikiwa zimeanzishwa na viongozi wanaoingia madarakani au wanaotaka kuingia madarakani. Ni awamu iliyopita tu ya braza Benny iliingia na "mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe". Na baada ya kitambo kidogo tu wasafiri wa mabasi kupitia Singida walivamiwa na majambazi na kuvuliwa nguo zao zote na kunyang'anywa kila kitu huku wakiimba, "mtaji wa Maskini ni nguvu zake mwenyewe".

Kwa kutafuta staili ya mtoko, JK naye akaona bora aandae falsafa yake ili aamushe hamasa miongoni mwa watanzania.Nakubali kwamba falsafa hizi zinatumiwa na mabwana hawa kwa nia nzuri, lakini watu walalahoi ambao wameona unyanganyi wa mali na roho za watu wasiokuwa na hatia ndiyo njia pekee ya kupambana na maisha ndani ya nchi inayopambana na janga la ukame na njaa.Sasa ni karibia matukio ya ujambazi ishirini yametokea, lakini lilotia fora ni lile la jana la NBC Bank pale karibu na Ubungo Plaza.Unajuwa ni mbinu gani iliyotumika?Ngoja nikusimulie kisa kilivyoanza.

Kama kawaida benki ni sehemu ambapo kila mtu anakwenda kuweka fedha yake au kuchukuwa fadha yake kwa matumizi mbalimbali.Wote tunalifahamu hilo na zaidi ya yote hata watu waweza kwenda pale kuomba mikopo ya kaanzishia biashara zao.Kuweka hela benki kwaweza kuwa ni sababu ya kiusalama, kuzibiti matumizi kwa watu wanaowashwa na fedha pindi ikiwa mfukoni na kupata riba kwa wengine. Kabla sijaenda mbali, kwanza ngoja niwarejeshe kwenye mbinu hiyo iliyokwapua mamilioni ya madafu yasiyofahamika idada yake na kutokomea hivi huku raia wakiona ni sinema ya "Holiwudi".Mbinu hiyo ni ya kishehe au Kiimamu,wale maswahiba wenzangu mwaweza kuwa mnawafahamu yakhe!Ni kwamba majamaa yaliingia na kanzu zao zilizopambwa na baraghashia utafikri yanatinga masjidi.Hii ni kali.Labda hapo baadaye yatamwiga padri au askofu.Ni katika hali hiyo bila kutegemea wateja wakaona gauni zile zimejifunguwa ghafla bini vu siraha za kila aina bastola, SMG n.k. Sasa hapo kilichofuta ni kusalimisha kilicho chao kama unataka uendelee kuvuta hii hewa na kusubiria kifo kilichopangwa na Allah.Ni katika hali hiyo pia majambazi hawa kwakatokea kama chui waliovaa ngozi ya chui kutawafanya vijana wa Mahita washindwe kuwadhibiti.

Mimi ni msomaje mzuri sana wa magazeti ya bongo kila siku.Lakini nilipopitia gazeti moja na kuona Mahita akitetea unga wake kwa kusema sasa vijana wake inabidi wazame striti ili wapambane na vijana wanaoiba kwa kutumia falsafa ya ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya. Mimi nilitamani watu wangempa mawazo huyu mzee namna ya kuwaimarisha hawa vijana wake. Jeshi la polisi linatakiwa kupewa elimu ya haki za binadamu pamoja na mbinu mpya za kupambana na uharifu. Nikimaanisha wajifunze zaidi nini wanachotakiwa kufanya ili kuondoa tatizo hilo sugu la ujambazi. Na vile vile wapewe siraha kubwa hasa maeneo ya taasisi za kifedha badala ya kukaa na virungu. Wajifunze namna ya kutafuta habari za majambazi hao ili wazuwia uharifu unaoweza kujitokeza.Hapa mbinu mpya zinatakiwa ziimarishwe pande zote za nchi hasa Dar.Kwa hali inayoonekana kukerwa na ujambazi, Mwamnyange naye kaja na njia nyingine ya kiini macho ati kufanya msako nchi nzima wa siraha zinazomilikiwa kiharamu.Kama inatangazwa kwamba watafanya msako wanafikiri wamiliki ni wajinga?Watahakikisha wamezificha zana zao za kazi.Napenda kuhitimisha kwa kuwataka wabongo wenzangu wawe macho pengine njia ya unabii hapo baadaye yaweza kutumika kuiba na hivyo kubaki swala la imani au kuabudu kukiwa ni tishio. Asalaam alaikum waallah matulallah wabaallahkatuh!

Wednesday, February 01, 2006

Salaamu kwa Wanablogu.

Asalaam alaikum ndugu zangu wananblogu!.Kama nilivyodokeza hapo jana ni kwamba nitakuwa nikiwaletea au nikiwadondoshea matone ya fikira kutoka katika kisima hiki ambacho kimechimbwa masaa kadhaa yaliyopita.Kama ilivyo jadi ya wanablogu kama Makene, Minja, Mwaipopo na Ndesanjo amabaye jitihada zake kuhakikisha vijana nasi tunakuwa "bloggerised",kama wenzetu hawa wenye ung'eng'e wanavyoweza kusema namshukuru sana kwani ameamsha baragumu.Baragumu nalo baada ya kupiga kwa mda mrefu kiu ikalikamata ikabidi nalo litafute kisima ili nacho kitowe maji ya kulainisha koo.Kwa mantiki hiyo basi, ni maji hayo hayo yatakayolainisha akili hasa za watanzania wenzetu waliolala ili waweze kufahamu yanayojili nje ya bongo kupitia blogu hizi.Nawaomba muendelee kuwapatia wenye kiu kisima hiki wakati huu wa ukame.Nawahi kuingia darasani nitawapasha habari zingine hapo baadaye.

Tuesday, January 31, 2006

Hala Hala Naja Bloguni


Nimekuwa nikisikia blogu na kelele nyingi zikija masikioni mwangu kuhusu huyu blogu ila sikuwa na shauku ya kuwa nayo.Hala hala sasa naja kwa kishindo nkitokea ndani ya barafu inayokaribia kunigandisha mapafu.Halafu kitu kingine kilichonizuwia ilikuwa ni staili ya kutoka na blogu hilo.Kelele za ndugu yangu Makene na Mnyambala Mwaipopo hatimaye zimefanikisha jukumu la uwanja wa pekee kuwapa mawazo.Haya karibuni tubadilishane mawazo kwa njia hii yenye uhuru wa kipekee.
Katika picha hiyo naonekana upande wa kushoto nyuma nikiwa nimevaa fulana nyeusi. Waliosimama kutoka nyuma na waliokaa kutoka kushoto ni Subira Kabula, Makene Boniphace na Clara Francis bila kumsahau mnyambala mwenzangu kutoka Mbeya tuliyesimama naye nyuma kwenye picha.Hawa wote ni walimu wa Kiswahili katika vyuo vikuu mbali mabali huku Marekani.