Thursday, February 23, 2006

Taswira ya Utamaduni wa Mwafrika.

Ilikuwa siku ya Jumatano tarehe 23, Februari hapa Illinois ndani ya Chuo cha Magavana ninapofundisha lugha ya kiswahili na utamaduni wa mtanzania nilipobahatika kujuwa nini utamaduni wa mwafrika kwa hawa wenzetu. Wakiwa na mabango makubwa kwenye malango ya chuo hiki niliona maandishi ya kiingereza yasemayo "African Cultural Heritage Day". Kusema kweli sikufahamu nini kinachoendelea juu ya hili.Baada ya kuonana na bosi wangu katika programu hii ya lugha za kimataifa, alinipokea kwa furaha huku akiniambia nisikose siku hiyo kuhudhuria kana kwamba angeweza kuniambia ni heri nikosa mguu mmoja badala ya kuikosa siku hiyo.Hapo ilikuwa siku moja kabla ya tarehe hiyo nilipotonywa na huyo mkubwa wangu.

Kwa bahati nzuri siku hiyo ilikwenda sambamba na siku ambayo mimi na mwenzangu kutoka Nigeria huwa tunakuwa na darasa la kufundisha Riwaya za Kiafrika au kama sikosei kwa king'eng'e inajulikana kama "Afrcan Novels". Kama kawa maprofu tulikusanya madesa yetu kuelekea kunako klasi huku tukitaraji kukuta madenti wakiwa wanatusubiria. Hamadi kuingia tukakuatana na ujumbe unaotuambia kwamba wamekwenda huko kwenye african cultural heritage na wangerudi ndani ya kitambo kifupi. Baada ya mda walirudi tukaendelea na darasa huku mwenzangu akichambua maudhui ya riwaya za kiafrika kwa kuelezea ni jinsi gani zilivyobadilika kulingana na wakati akimaanisha kabla ya ukoloni , wakati wa ukoloni na baada ya ukoloni. Wakati wa mapumziko kama ilivyo ada ya ufundishaji wa huku, mkuu wetu akashauri twende kwenye manesho hayo tuyarishe macho yetu urithi wa utamaduni wa mwafrika.

Asalale!Nilipigwa na bumbuwazi kukuta maonesho hayo yametawaliwa na picha za kizamani. Nyingi yazo zikiwa ni zile zilizopigwa na "manthropolostisi" kabla ya mwaka 1935.Picha hizo zilimwonyesha mwafrika wa kike kwa dharau sana huku matiti yake yakiwa nje na sehemu zake nyeti zikiwa zimefunikwa na kipande cha ngozi. Wanawake wengine walionekana wakiwa na nyuso zilizopakwa rangi na kuchanjwa au kutengeneza michirizi usoni mwao na mwili mzima. Ndugu zangu wasomaji ni kwamba picha hizo zote zinaonekana kuchukuliwa kutoka eneo moja la afrika ya kati hasa Congo Brazzaville (Kongo kwa sasa) na Congo Kinshasa(Zaire au DRC kwa sasa). Kama ilivyo ada ya hawa wenzetu na uwezo wao mdogo wa kufahamu nini kinachoendelea nje ya nchi hii walianza maswali mbali mbali ya kutaka kufahamu nini hasa kinaendelea maeneo haya. Rafiki yangu kutoka Nigeria alikuwa wa kwanza kuulizwa swali akasema kwanza hizi picha si za kweli inaonekana mtu aliwalazimisha kujiandaa kupiga picha ukizingatia kilikuwa kipindi cha ukoloni. Akwaambia ona msichana huyu anavyoangalia, unaona kwamba kabisa anaambiwa na mtu mbele yake kaa hivi. Mimi nikaongezea kwa kusema, picha hizi zimetoka katika sehemu moja ya Afrika japokuwa siamini kama ni za kweli, ila ninachofahamu hamwezi kujumuisha mambo kwa kutumia nchi mbili tu.Hii yote ni kupotosha utamaduni wa bara zima kwa kuleta picha na vitu vinavyowaonyesha wakiwa uchi tu.

Baya zaidi ni hawa wenzangu weusi walionitangulia kuja huku. Eti Afican-Americans?Mimi na wao tunatofautishwa na mda tu. Wao babu zao walikuja wakiwa wamepangwa kwenye majahazi kama nafaka na mimi nimekuja kwa hiari tena ndani ya ndege.Lakini ukiangalia walivyokuwa wanadhihaki na kushangaa hizo picha utafikiri wao hawakutokea huko.

Baada ya matembezi hayo tulirudi darasani kuendelea na kipindi.Kabla ya hapo, tukaongelea ju ya maonesho hayo huku huyo profesa mwenye asili ya kiafrka na anayeonekana kuelewa asili yake akisema kuwa huwezi kusema ndivyo ulivyo utamaduni wa mwafrika kwa ujumla.Akasema huo ni upotoshwaji wa utajiri wa utamaduni wa mwafrika.Hii ilinikumbusha niliposoma kwenye blogu ya Jeff na hasa makala ya jamaa mmoja anaitwa Wainaina niliona mtazamo wa hii mijitu juu ya bara letu. Kwa hiyo nami nilimweleza rafiki yangu kwamba ndiyo maana tulipokwenda kutembelea Museum moja mjini Chicago kwa upande wa Afrika tuliona wanyama tu na sehemu kidogo ya mapishi vikiwa ndo viwakilishi vya tamaduni za bara letu.Nilipojaribu kuowanisha na makala hiyo nikajiuliza,watu hawa wanapeleka wapio utamaduni wetu?Nini hasa chanzo cha uharibifu wa utamaduni huu mzuri na wa aina yake?Na lini hawa watu wataacha kuharibu mama wa ustaarabu wa mwanadamu hasa mbele ya hiki kizazi chao chenye laana?

Asalaam alaykum!.

5 Comments:

At 2:32 PM, Blogger John Mwaipopo said...

Haya ndio mauzauza. Mwalimu wangu wa hapa chuoni husema kuwa "History is written by the winners." Nimeona niweke kizungu kwa kuchelea kupotosha maana kwa tafsiri yangu. Waswahili wa marekani (Afro-Americans) wamelishwa sumu kuwa waswahili wa Afrika (akina siye)tuliwauza na ndio chanzo cha utumwa wao. Hebu fikiria umuuze ndugu yako! Au kulikuwa na aina fulani ya shinikizo kutoka kwa wazungu.

Ninachotaka kusema hapa ni kuwa sumu waliyolishwa hawa waswahili wa marekani imewafanya hata wasijisumbue kutafuta na kusoma asili yao. Hata haya ya picha wanaletewa na mzungu huyo-huyo. Yeye ndiye anaamua aendelee kuwalisha sumu gani. Hakika wana kitambo mpaka hapo watakapoelewa ukweli.

Hata hivyo, hivi kule Bongo sehemu za 'Ntwara' wamakonde nao sio wamejichana chale usoni na kadhalika. Hivi wachagga na watu fulani mikoa ya katikati na Musoma huko wameshaacha kukeketa (kutahiri) wanawake. Nasi waswahili wa afrika kuna viutamaduni tunatakiwa tujifunze kuviacha. Ndivyo hivi hawa wazungu huchukulia kama generalization ya bara zima la Afrika.

 
At 5:28 AM, Blogger msangimdogo said...

Tatizo kubwa hapa ni kutojitambua na wala sio kulishwa sumu ya aina yoyote ile, kwasababu kama ni suala la sumu tayari tulishakunywa na imeanza kutukoroga matumboni, sasa kwanini tuhangaike kutafuta maziwa haraka haraka wakatu tunajua wazi kuwa tulinyweshwa sumu? Kama tungalikuwa hatujui sawa, lakini midhali tunajua.....

 
At 7:11 AM, Blogger Maricha said...

john Mwaipopo taratibu kaka mbona unatusakama tunaokeketa? swala hapa halikuw akuhusu kukeketa wala bwana January hakusema zimewekwa picha za kukeketa.

Kwa mtizamo wangu sioni ubaya wa hao wazungu kuweka hizo picha za wanawake walioficha utupu wao tu na kuacha maungo yaoi mangine wazi, wala hazinisumbui hizo picha kwani hadi leo kule Tanzania sehemu nyingi za afrika wanawake kuacha maziwa wazi sio bigi dili.

Kitu nnachokiona sio kyema kutokana na maelezo ya January ni kutoweka picha zilizo uptodate zinahusu afrika kwani wangekuwa na picha at least ya kila muongo, hio ingeonesha ni jinsi gani utamaduni wetu umeenda ukibadilika na kukua au kufa.

Unajua sie wakurya tunatoboa maskio wake kwa waume, tena tuulikuwa tunatoboa hadi yana ninginia. nna picha za babu akiw ana maskio yananing'inia sioni haya wala shemu kwa hilo na picha nimezibandika home kwangu na kwene alubamu zangu. kwahiyo nikiona vijana wanatoboa maskio siku izi wala sishangai kwani wanaiga utamaduni wa mwafrika woote akina maiko joridani nikiwaona na vehereni vyao naona wanaiga utamaduni wetu na naona masifa sana

 
At 6:40 PM, Blogger barb michelen said...

Hello I just entered before I have to leave to the airport, it's been very nice to meet you, if you want here is the site I told you about where I type some stuff and make good money (I work from home): here it is

 
At 2:09 PM, Blogger bernard n. shull said...

i did a little research after you told me about your "thing", and if you want a way to make more money using your your blog you can enter this site: link. bye.

 

Post a Comment

<< Home